SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

OFISI YA RAIS KATIBA, SHERIA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA

MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Haroun Ali Suleiman, leo tarehe 11 Juni 2026 amefanya mkutano na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Sheria House, Mazizini Zanzibar, kwa lengo la kutoa taarifa kuhusu Uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili (MSLAC II). Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Waziri amesema uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika tarehe 20 Juni 2026 katika Viwanja vya Maonesho Dole–Kizimbani, ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ameeleza kuwa katika awamu ya kwanza ya kampeni hiyo, kwa upande wa Zanzibar, Kampeni hii ilizinduliwa katika Mikoa mitatu ya Zanzibar, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mkoa wa Kusini Unguja na Mkoa wa Kusini Pemba ambapo jumla ya Wananchi waliofikiwa ni 422,908 wanaume ni 213,723 wanawake 209,185 kutoka katika Halmashauri, Wadi na Shehia mbali mbali za Unguja na Pemba. Mhe. Dkt. Haroun ametoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi kushiriki kampeni hiyo ili kupata elimu ya kisheria, kuwasilisha changamoto zinazowakabili na kupata huduma stahiki kutoka kwa wataalamu wa sheria na taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za haki. Kauli Mbiu: “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo.”