UZINDUZI WA MFUMO WA CIVIL SERVANTS' MANAGEMENT SYSTEM (CSMS)
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Dkt. Haroun Ali Suleiman amesema kuanzishwa kwa Mfumo wa Usimamizi wa Watumishi Serikalini (Civil Servants Management system - CSMS) kutasaidia kuimarisha ufanisi wa utendaji kazi, kuongeza uwazi na kuhakikisha Serikali inakuwa na taarifa sahihi za watumishi wake. Alisema mfumo huo ni muhimu katika kukabiliana na changamoto ya kutokuwa na taarifa kamili za watumishi, ikiwemo wale wanaokwenda masomoni nje ya nchi bila taasisi zao kuwa na taarifa sahihi kuhusu maendeleo yao ya masomo na muda wa kurejea kazini. Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mfumo huo, Dkt. Haroun alisema kumekuwa na changamoto ya baadhi ya viongozi kutofahamu idadi na taarifa za watumishi waliopo katika taasisi zao, hali inayoweza kuathiri usimamizi na upangaji wa rasilimali watu. Alisema ni jambo la lazima kwa kila kiongozi wa taasisi kufahamu idadi ya watumishi alionao, sifa zao za kitaaluma, majukumu yao na muda uliobaki kabla ya kustaafu, ili kurahisisha maamuzi na kuimarisha utendaji wa taasisi. Waziri Haroun alisema mifumo ya kidijitali inayowekwa serikalini haipaswi kuwa mapambo ya ofisi, bali inapaswa kutumika kikamilifu katika kurahisisha kazi na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma. Alisisitiza umuhimu wa ufuatiliaji wa mifumo hiyo baada ya kuanzishwa kwake, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuhakikisha inafanya kazi kwa malengo yaliyokusudiwa. Aliwataka wakurugenzi wa utumishi na viongozi wa taasisi za Serikali kuhakikisha wanatumia mifumo hiyo ipasavyo na kuwapatia watumishi elimu inayohitajika ili waweze kuendana na mabadiliko ya teknolojia, ikiwemo matumizi ya akili unde (AI). Dkt. Haroun alisema elimu hiyo itasaidia watumishi kutambua taarifa sahihi na zisizo sahihi, hasa katika kipindi ambacho teknolojia inaweza kutumika kutengeneza taarifa zinazoweza kupotosha ukweli. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuweka utaratibu madhubuti wa kuhakiki vyeti vya elimu, vyeti vya kuzaliwa na taarifa nyengine za watumishi ili kubaini uhalali wake na kukabiliana na udanganyifu unaoweza kujitokeza katika ajira na utumishi wa umma. Alisema mifumo hiyo inapaswa kusaidia kubaini watumishi wanaokaribia umri wa kustaafu kwa kuzingatia taarifa sahihi na taratibu za kisheria, ili kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa masuala ya utumishi. Katika hatua nyingine, Waziri huyo alitoa tahadhari kwa watumishi wanaoishi katika maeneo hatarishi, hususan maeneo ya mabondeni, kuchukua tahadhari na kuanza kujiandaa kuhama mapema endapo watapewa taarifa za uwezekano wa kutokea kwa mafuriko kutokana na mvua zinazotarajiwa. Awali, Katibu wa Tume ya Utumishi Serikalini Bi. Zaituni Mohammed Haji, alisema mfumo huo umeandaliwa kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utumishi wa umma bila kubadilisha sheria na kanuni zilizopo zinazosimamia masuala ya utumishi. Alisema miongoni mwa malengo ya mfumo huo ni kuiwezesha Serikali kufahamu idadi kamili ya watumishi, kuimarisha michakato ya usimamizi wa rasilimali watu, kupunguza matumizi ya kazi za mikono na makosa yanayoweza kufanywa katika uingizaji na usimamizi wa taarifa za watumishi. Aliongeza kuwa mfumo huo utaimarisha uwazi na upatikanaji wa taarifa sahihi kwa matumizi mbalimbali ya kiutumishi, huku kila mtumishi akiwa na akaunti yake binafsi itakayomwezesha kupata taarifa zake. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Rasilimali Watu, Utawala na Mipango (e-GAZ) Nd. Ashraf Mohammed Abdalla akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Zanzibar (e-GAZ), alisema mamlaka hiyo inaendelea kuunganisha mifumo ya Serikali ili kuimarisha utoaji wa huduma na kurahisisha utendaji kazi. Alisema hatua hiyo ni muhimu katika kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma, hususan katika upatikanaji wa huduma na uwasilishaji wa maombi na nyaraka mbalimbali ambazo hapo awali zilichukua muda mrefu kushughulikiwa. Alieleza kuwa Serikali inaendelea na azma ya kuunganisha mifumo yake kupitia ZanExchange, hatua itakayowezesha taasisi kubadilishana taarifa kwa njia ya kidijitali na kupunguza ulazima wa wananchi kutoa taarifa zilezile wanapohitaji huduma katika taasisi tofauti. Alisema lengo la muda mrefu ni kuelekea katika mfumo wa ZanPortal, utakaowezesha wananchi kupata huduma mbalimbali za Serikali kupitia kiunganishi kimoja cha mtandao. Naye Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Rasilimali watu katika Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Nd. Bakari Khamis Muhidini alisema awali Serikali ilikuwa na mfumo wa mishahara pekee, ambao ulikusanya taarifa za watumishi lakini haukuwa na uwezo wa kutosha wa kuzichakata kwa ajili ya kupata takwimu zinazohitajika katika maamuzi ya kiutumishi. Alisema Serikali imeendelea kufanya uimarishaji ya mifumo iliyopo na kuanzisha mingine ili kuhakikisha taarifa za watumishi zinapatikana kwa urahisi na kutumika katika kupanga mahitaji ya rasilimali watu. Alitaja miongoni mwa mifumo inayotarajiwa kuanzishwa kuwa ni Mfumo wa Mafunzo ya Watumishi, utakaosaidia kufuatilia watumishi wanaokwenda masomoni, muda wa mafunzo yao na tarehe za kurejea kazini. Mifumo mingine ni wa kupima utendaji kazi wa watumishi kwa njia ya kielektroniki (PEPMIS), mfumo wa leseni na vibali vya kazi pamoja na mfumo wa kushughulikia kero za watumishi. Alisema pia mfumo wa maombi ya ajira unafanyiwa maboresho kuelekea awamu ya tatu ili uweze kuchakata maombi badala ya kuyakusanya na kuyahifadhi pekee kama ilivyokuwa awali. Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi Serikalini, Dkt. Idrissa Muslih Hija, alisema wajumbe wa tume hiyo watahakikisha mfumo huo unasimamiwa ipasavyo ili ufanye kazi kulingana na malengo yaliyowekwa. Alisema tume imekuwa ikishuhudia changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya utumishi wa umma, hivyo anaamini matumizi ya mfumo huo yatasaidia kurahisisha shughuli za kiutumishi na kuimarisha usimamizi wa watumishi. Kwa upande wake, Meneja Muendeshaji wa kampuni ya Web Technologies Nd. Mandaro Juma Mandaro, alisema kampuni hiyo iliyoshiriki kuandaa mfumo huo inaamini utaleta tija katika utendaji wa Serikali na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Alisema matumizi ya mfumo huo yataongeza ufanisi wa kazi na kusaidia upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wakati unaohitajika, hatua itakayorahisisha shughuli za kila siku za watumishi wa umma.