SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR IMEPOKEA MSAADA WA TANI 20 ZA TENDE KUTOKA KAMPUNI YA KING SALMAN HUMANITARIAN AID AND RELIEF CENTER KWA AJILI YA WANANCHI WA ZANZIBAR
Saudi Arabia na Zanzibar ni nchi ambazo zimekua na mashirikiano ya muda mrefu ambayo yamepelekea kukua kwa mahusiano ya Kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili katika maeneo mbali mbali ikiwemo masuala ya kiuchumi, kiutamaduni na kijamii. Ameyasema hayo Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora anayeshughulikia masuala ya Katiba na Sheria, Ng. Mzee Ali Haji wakati wa hafla ya makabidhiano ya msaada wa tani 20 za tende uliotolewa na Kampuni ya King Salman Humanitarian Aid and Relief Center ya Saudia Arabia kwa ajili ya wananchi wa Zanzibar.chini ya Uongozi wa mfalme Salman bin Abdulazizi Al Saud ulio wakilishwa na mwakilishi wa Kampuni hiyo ndugu Abdallah Al-Twaiby. Naibu Mzee ameeleza kuwa msaada huo ni ishara ya muendelezo wa mahusiano mazuri kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Saudi Arabia uliopo kwa kipindi kirefu na juhudi hizo zinaunga mkono dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kuwa wananchi wa Zanzibar wanafikiwa vyema katika kuimarisha huduma zao za kijamii. Aidha, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa washirika mbalimbali wa maendeleo na taasisi za kibinadamu ili ziweze kutekeleza shughuli zao kwa ufanisi na uwazi. Hafla hiyo imefanyika leo tarehe 28 Julai, 2026 katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora iliyopo Mazizini, Zanzibar.